Mkutano Mkuu wa Kitaifa wa 63 wa Jumuiya ya Wabahá'í wa Tanzania ulifanyika kwa mafanikio makubwa tarehe 24—26 Aprili 2026 katika Kituo cha Wabahá'í, Upanga — Dar es Salaam.
Mkutano huo uliwakutanisha zaidi ya marafiki 80, wakiwemo wawakilishi kutoka jamii mbalimbali za Wabahá'í nchini, Mshauri wa Bara, Bw. Agustino Ibrahimu, Washauri Wasaidizi, pamoja na wageni waalikwa.
Kati ya wawakilishi 57 waliochaguliwa katika hatua za awali za mchakato wa uchaguzi, asilimia 98 walishiriki kikamilifu katika upigaji kura. Ushiriki huu mkubwa unaonesha kiwango cha juu cha ukomavu, kujitolea na uelewa wa umuhimu wa mchakato wa uchaguzi katika maisha ya Jumuiya ya Wabahá'í.
Miongoni mwa mambo muhimu yaliyojiri katika mkutano huo ilikuwa ni uchaguzi wa wajumbe wa Baraza la Kiroho la Kitaifa la Wabahá'í wa Tanzania kwa kipindi cha 2026—2027. Wajumbe waliochaguliwa ni:
Bw. Dunstan Ruta
Bw. Geofrey Nduke
Bw. Christopher Stevenson
Bi. Ester Mtisya
Dkt. Ola Johnpour
Bw. Gershom Mpumbiye
Bi. Suzan Kyando
Bw. Cleophace Ndaro
Bw. Samson Rutebuka
Aidha, washiriki walipata fursa ya kusoma, kutafakari na kujadiliana kwa kina Ujumbe wa Riḍván 2026, pamoja na barua ya tarehe 31 Desemba 2025 kutoka Nyumba ya Haki ya Ulimwengu. Nyaraka hizi zilitoa mwanga kuhusu kukamilika kwa awamu ya kwanza ya Mpango wa Miaka Tisa na kuanza kwa awamu ya pili ya mpango huo.
Mkutano pia ulipokea na kujadili ripoti ya utendaji ya mwaka 2025—2026, iliyowasilishwa na Katibu wa Baraza la Kiroho la Kitaifa. Majadiliano haya yalitoa fursa ya kutathmini maendeleo yaliyopatikana, changamoto zilizojitokeza, pamoja na maeneo yanayohitaji kupewa kipaumbele katika kipindi kijacho.
Tunawapongeza kwa dhati wajumbe wote waliochaguliwa na tunawatakia mafanikio mema katika kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, bidii, unyenyekevu na moyo wa huduma kwa jamii ya wanadamu.
Tunatoa pia shukrani kwa washiriki wote, wawakilishi, Washauri, wageni waalikwa na wote waliochangia kufanikisha Mkutano Mkuu wa Kitaifa wa 63.
Maoni (0)
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kutoa maoni.
Acha maoni