Katika kujenga maendeleo ya kweli na endelevu duniani, usawa kati ya mwanamke na mwanaume ni msingi muhimu usioweza kupuuzwa. Kadiri jamii inavyoendelea kutambua, kuthamini na kuwezesha nafasi ya mwanamke, ndivyo uwezo wake wa kuchangia katika maendeleo ya familia na jamii unavyozidi kudhihirika.

Kwa muda wa siku tatu, wanawake walikutana katika kongamano maalumu la kutafakari, kujifunza na kushauriana kuhusu namna wanavyoweza kuimarisha na kuongeza mchango wao katika maendeleo ya familia na jamii. Katika kipindi chote cha kongamano, washiriki walijifunza Maandiko Matakatifu pamoja na jumbe za Nyumba ya Haki ya Ulimwengu kuhusu nafasi na mchango wa wanawake katika maendeleo ya familia na jamii.

Mojawapo ya uelewa muhimu uliojitokeza kwa kina ni kwamba familia ndiyo msingi wa kujenga jamii yenye maadili, umoja na maendeleo endelevu. Ilisisitizwa kuwa kila nyumba inaweza kuwa kitovu cha ibada, mazungumzo yenye kujenga, huduma kwa wengine, pamoja na shughuli mbalimbali za kielimu zinazotolewa kupitia taasisi za mafunzo.

Washiriki pia walitafakari umuhimu wa makundi ya familia kama njia madhubuti ya kupanua ushiriki wa watu binafsi na familia katika mchakato wa kujenga jumuiya imara na yenye uwezo wa kujifunza. Kupitia makundi haya, familia huimarisha urafiki, hujifunza pamoja na kushiriki katika shughuli zinazokuza maendeleo ya kiroho na kijamii.

Aidha, kongamano lilisisitiza nafasi muhimu ya akina mama kama walimu wa kwanza wa watoto. Ilibainika kuwa wanawake wana mchango wa kipekee katika kujenga msingi wa maadili mema, tabia njema na maisha ya kiroho ya watoto na vijana. Uelewa huu umeongeza dhamira ya kuendeleza programu za kielimu na kuimarisha ushiriki wa familia katika malezi na makuzi ya kizazi kijacho.

Mwisho wa kongamano, washiriki waliondoka wakiwa na hamasa mpya na dhamira ya kuendelea kuimarisha familia zao, kushiriki kikamilifu katika shughuli za ujenzi wa jumuiya na kuwa chachu ya maendeleo katika maeneo wanayoishi.

Ujifunzaji uliopatikana umeweka msingi muhimu wa kuendeleza jamii zenye umoja, maadili na uwezo wa kuwalea watoto na vijana katika mazingira yanayokuza utu, huduma kwa wengine na maendeleo endelevu.