Baadhi ya wazazi katika jamii ya Msasani, Dar es Salaam, walikutana tarehe 7 Novemba 2026 kwa ajili ya kujadiliana kuhusu maendeleo ya vijana wao, kufahamishwa kuhusu shughuli mbalimbali za jumuiya na kutafakari namna wanavyoweza kushiriki kikamilifu katika kuunga mkono juhudi za maendeleo ya vijana chipukizi.

Katika mkutano huo, wazazi walipata fursa ya kusikia tathmini ya maendeleo ya kitaaluma ya vijana wao, kushauriana kuhusu hatua zinazofuata katika utekelezaji wa programu inayoendelea, pamoja na kubadilishana mawazo kuhusu namna ya kuimarisha ushirikiano kati ya wazazi na wale wanaowezesha programu hiyo.

Kwa sasa, katika ujirani huu kuna zaidi ya vijana chipukizi 60 wanaoshiriki katika programu ya masomo ya maandalizi ya kujiunga na kidato cha kwanza (Pre-Form One). Sambamba na masomo hayo, vijana wanajifunza vitabu vya programu ya uwezeshaji wa kiroho wa vijana chipukizi na kushiriki katika shughuli mbalimbali ambatanishi zinazosaidia kuimarisha ujifunzaji wao.

Juhudi hizi zinalenga kuwawezesha vijana chipukizi kukuza uwezo wao wa kiakili na kiroho, kujenga misingi imara ya kimaadili, na kuimarisha uwezo wao wa kuwa washiriki wenye tija katika maendeleo ya jamii zao.

Mkutano huu ulikuwa fursa muhimu ya kuimarisha uelewa wa wazazi kuhusu programu na nafasi yao katika kuunga mkono ukuaji wa vijana. Ushirikiano kati ya wazazi, wawezeshaji na jumuiya kwa ujumla ni sehemu muhimu katika kujenga mazingira yanayowawezesha vijana chipukizi kukua, kujifunza na kutumia uwezo wao kwa manufaa ya jamii.